Sunday, February 10, 2008

Mipango ya maisha yenu ya baadaye

Habari za leo?

Baada ya mjadala kuhusu hali ya kisiasa nchini Kenya pamoja na umuhimu na ongezeko la athari za Uchina ulimwenguni, nataka tugeukie swala tofauti linalohusiana na maisha yetu. Mimi napanga kurudi Kenya na kutoa mchango wamgu katika kufundisha. Aidha, nadhani nitafurahi mno ikiwa nitawza kuanzisha shule ya kuwasaidia vijana chipukizi kupata elimu nzuri. Tayari mimi nina mke na mtoto mmoja na napanga kupata wengine. Ningependa kujua mipango yenu ya baadaye maishani (baada ya Stanford). Zingatieni maswala kama masomo, kazi, familia, sehemu ya kuishi na kadhalika.

2 comments:

Daudi said...

Ninatarajia kwamba nitapata shahada yangu ya kwanza ya chuo kikuu hiki mwaka elfu mbili na kumi na watu wengi husema kwamba maisha yanaanza kwa kweli wakati unapokamilisha masomo.
Nitahitimu miaka miwili kabla ya michezo ya Olympiki kule nchini Uingereza kwa hivyo natarajia kwamba nitaendelea kuogelea kwa mashindano nitakapomaliza masomo yangu mpaka michezo hiyo. Halafu, nitapaswa kuamua kama ningetaka kustaafu au kuendelea kuogelea na ninafikiri swala hili litategemea kama uogeleaji bado utanifurahisha na kama nitaweza kuishi vizuri na pesa nitazopokea kutokana na mapato yangu.

Lakini ninayakini kuhusu kitu kimoja ambacho ni kwamba nitahitaji kupata kazi za halisi baada ya michezo na hiyo ni sababu kuwa ninasoma sasa hivi. Kazi maalum inayonifurahisha ni kazi kuhusu uchumi na fedha. Msemo maarufu katika Kiingereza ni kuwa ‘pesa inazungusha dunia’ na kwa maoni yangu ni kweli. Nilipokuwa mdogo daima nilitaka kujua mbona baadhi ya watu ni watajiri na wengine ni waskini. Bila shaka nataka kurudi nchini Kenya na nadhani kwamba nitajaribu kusaidia kukuza uchumi wetu ili raia waweze kuishi bora. Jinsi nzuri ya kusaidia watu pamoja na uchumi ni kupatia wanabiashara wadogo msaada mwendelevu bila ya kuwapatia pesa tu. Nilitazama mradi mmoja ya rafiki ya babangu ambaye alikuwa anasaidia wakulima wa (avocadoes) kushirikiana ili waweze kuuza mazao yao moja kwa moja kuuzwa ng’ambo kwa bei nafuu kuliko zamani. Mabadaliko madogo kama haya yalisaidia kiasi cha kwamba jamii yote ya kijiji hicho iliathiriwa na watu waliweza kuishi bora zaidi.

Kuhusu familia, mimi ni kijana tu kwa hivyo sina mpango wa familia lakini nikikutana na msichana mmarekani na kutaka kumwoa angehitaji kuhama kuelekea Kenya kwa sababu sitaki kubaki hapa Marekani kwa maisha yangu yote.

Jason said...

Baada ya masomo yangu ambayo nitamaliza mwaka ujao, nina hamu ya kuingia dunia ya uogeleaji wa kucheza kwa mshahara (professional?) angalau mpaka mwaka wa elfu mbili kumi na mbili. Halafu nitakapofika mwaka huo, iwapo nitakuwa nikifaulu katika Michezo ya Olimpiki, na kuwa nikipata pesa ya kutosha labda nitaendelea hadi wakati ambao mwili wangu utaniambia kukoma kuuadhibu.

Kwa kweli mbali na uogeleaji sijui aina ya kazi ningetaka kufanya katika maisha yangu ila ninajua kwamba nitarudi Kenya na nitashughulukia katika kazi ya mazingira au ya michezo. Katika maisha yangu ningetaka kuhisi kwamba nimejitahidi kusaidia watu ambao wanaishi katika unyonge ili waishe maisha nafuu bila kuathiri mazingira yao vibaya. Kufaulu katika ndoto hii hakutakuwa rahisi lakini kama methali inatuambia “penye nia pana njia.” Mimi nina nia kubwa ya kufanya kazi hii, swala ni kutafuta njia mwafaka zaidi.

Kuhusu familia yangu na ningetaka kulea watoto wangu nchini Kenya, pamoja na kuishi na mke mrembo humo. Wakati huu nina mpenzi Mwamerika wa zaidi ya miaka miwili ambaye ninaabudu sana. Mwaka uliopita alinitembelea nchini Kenya, tulisafiri kote nchini na aliipenda nchi yetu sana. Ameniambia kwamba ikiwa siku moja nitamwoa, hatakuwa na matatizo ya kuhamishwa kuishi Kenya pamoja nami, kwa hivyo nadhani kwamba nina baraka nyingi!